Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahl al-Bayt (AS) - Abna, Waziri wa Mambo ya Nje wa Imarati alikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kizayuni huko Abu Dhabi siku ya Jumapili, na katika kikao hiki walijadili "kustawisha uhusiano" kati ya nchi hizo mbili na kuhalalisha kile kinachoitwa Uhusiano wa kawaida Kati ya Israel na nchi za Kiarabu (Arab - Israel Normalization).
Mkutano huu ulifanyika wakati Israel inaendelea kuwaua Wapalestina huko Gaza na hali ya kibinadamu katika eneo hili ni mbaya sana.
Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Emirates (WAM), Abdullah bin Zayed alijadili uhusiano wa nchi mbili na maendeleo ya hivi karibuni katika maeneo ya kikanda wakati wa mkutano huu akiwa na mwenzake Sa'ar. Katika mkutano huu, suala la Gaza na juhudi za kurejesha usitishaji mapigano pia zilijadiliwa.
Katika kikao hicho, Waziri wa Mambo ya Nje wa UAE amesisitiza umuhimu wa kujaribu kufikiwa usitishaji vita na kuachiliwa huru wafungwa na kusema: Ni lazima tuzuie kuenea kwa migogoro katika eneo. Vile vile amesisitiza uungaji mkono wa Imarati kwa juhudi zote za kidiplomasia za kuwalinda raia na kuimarisha hatua za kukabiliana na mzozo wa kibinadamu huko Gaza. Bin Zayed aidha amesisitiza ulazima wa kuundwa kwa upeo mkubwa wa kisiasa kwa ajili ya kuanzishwa tena mazungumzo baina ya israel na Hamas ili kupatikana amani ya kudumu yenye msingi wa Muungano wa nchi mbili Israel na Palestina, na kutoa wito wa ushirikiano wa jumuiya ya kimataifa ili kukidhi matakwa ya wananchi katika uga wa usalama na utulivu.
Waziri wa Mambo ya Nje wa UAE pia ameashiria hali ngumu ya raia huko Gaza na kusema: Hali hii inahitaji juhudi za kila upande ili kuhakikisha mtiririko wa misaada ya kibinadamu kwa njia salama na shwari bila kuwepo vikwazo. Amesisitiza ulazima wa ushirikiano wa kieneo (kikanda) na kimataifa ili kukabiliana na misimamo mikali na chuki na kutoa wito wa kukuzwa thamani za kuishi pamoja na udugu wa kibinadamu katika eneo hilo la kikanda (Yaani: Mashariki ya Kati).
Mwezi uliopita, UAE ilikuwa mwenyeji wa wakuu kadhaa wa makazi ya walowezi wa Israeli, ambayo inaonekana kama hatua mpya kuelekea kuhalalisha uhusiano wala Israel na Imarati. Kuhusiana na hili, gazeti la Yediot Aharonot liliripoti kwamba viongozi hawa walisafiri hadi Abu Dhabi ili kufuturu kwa mwaliko wa Ali Rashid Al Nuaimi, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi, Mambo ya Ndani na Nje ya Baraza la Kitaifa la UAE.
Viongozi wa walowezi wa Israeli wanaamini kuwa kipindi hiki "kinaleta fursa za kihistoria za kuhalalisha mahusiano ya kawaida ambazo hazipaswi kukosekana." Kuhusiana na hili, Mkuu wa Baraza la Yeshua, Yisrael Gantz, alisema: "Mpangilio mpya wa ulimwengu unahitaji ushirikiano mpya na kufikiri nje ya sanduku." Safari hiyo ilijumuisha kukutana na maafisa wa Serikali ya UAE, wafanyabiashara na washawishi, pamoja na kukutana na balozi wa Israel katika nchi hiyo ya UAE, Yossi Shili.
Your Comment